![]() |
| Picha: Getty images/ Andrew Bret Wallis |
Kifo ni fumbo la imani kama inavyopendwa kunukuliwa na viongozi wa dini: maadamu tu hai basi kufa lazima. Kifo kimeumbwa kwa ajili yetu bin Adam na kitakoma tu, pale siye wote wana wa Adamu tukiwa tumefutika katika uso wa dunia..
Tupatapo misiba huwa mara nyingi hali ya kuhamanika hutujia, mawazo na fikra mbalimbali hushamiri mpaka muda mwingine zinatupelekea kumkufuru Mola wetu Jalia.
Hali ya kuhamanikia hutokea kwa sababu ya mshtuko mkubwa wa kihisia, huzuni kali, na maumivu ya kupoteza mtu muhimu katika maisha yetu. Hofu ya kukosa udhibiti wa hali, kutokuwa na uhakika kuhusu maisha bila wao, na upweke wa ghafla unaweza kuongezeka, na kusababisha wasiwasi uliopitiliza na kuhamanikia.
Bi. Polina Maranova mmiliki wa Waraka wa Habari uitwayo ‘The Profile’, na pia Polina ni muandishi wa kitabu cha ‘Hidden Genius’. Katika waraka wake wa Agosti, 21 mwaka huu ulioenda kichwa cha Waraka: 'My Annual Birthday Check-In: 11 Lessons From 33 Years on This Planet’. Katika Waraka huo allkuwa anatushirikisha mafunzo kumi na moja ya maisha katika miaka thelathini na tatu — kwenye funzo la sita alizojifunza ndani ya miongo mitatu ni kuwa: “Hadithi zote za mapenzi zimetarajiwa kumalizika kwa msiba (Tragic loss).” kwenye kulichambua funzo la maisha alisema alishawahi kumsikia mwandishi Nicholas Sparks (ni muandishi gwiji wa riwaya kubwa nne ambazo anaelezea misiba mizito (Tragic loss) ya visa vya mapenzi; The Notebook, A Walk to Remember, Dear John, na A Message in a Bottle) akisema haya kwenye mahojiano:
"Kwangu, mapenzi na msiba vimeungana. Huwezi kuwa na moja bila jingine. Na kadiri mapenzi yanavyokuwa makubwa, ndivyo msiba unavyokuwa mkubwa zaidi.”
"Unaona, kila siku mamilioni na mamilioni ya watu ulimwenguni wanakufa, na sisi sote tunaendelea na maisha yetu, tunakwenda kazini, hatujali. Lakini pale inapokuwa ni mtu unayempenda — dada yako, mke wako, babu au nyanya yako, rafiki yako — ni kama dunia yako inaanguka. Na kadiri mapenzi yalivyokuwa makubwa, ndivyo msiba unavyokuwa mkubwa zaidi.
"Hivyo basi, kwa tafsiri, hadithi zote za mapenzi lazima ziishie kwa msiba."’
Nazidi kujazia nyama kwenye mantiki hiyo ya ‘hadithi zote za mapenzi lazima ziishie kwenye hali ya msiba’. Kwahiyo ilimradi tu kuna upendo, hakutakosa kuwa na huzuni. Huzuni ya wakati uliopita; ya maisha kuendelea na ombwe la nafasi tupu ambalo zamani lilijaa vicheko, furaha, kuthaminiana, amani na nguvu za watu tuliowapenda.
Kwenye upendo uliokithiri wa ndugu, jamaa, wenzi na rafiki unaweza kumithililisha na bustani yenye maua ya aina nyingi. Upendo wa watu wa karibu ni kama miti yenye mizizi imara, inayotupa kivuli na utulivu, ikitufanya tuhisi tuna ulinzi na msaada wa kudumu. Upendo wa wenzi ni kama waridi wenye harufu nzuri na rangi angavu, unaotuletea furaha ya kipekee, shauku, na utamu wa mapenzi. Upendo wa marafiki ni kama maua ya porini yanayochanua kila kona, yakijaza bustani yetu na rangi za furaha, kicheko, na urafiki wa kweli. Bustani hii ya upendo ina aina mbalimbali za uzuri, kila moja ikiongeza thamani ya kipekee na kutufanya tuhisi tumezungukwa na furaha, nguvu, na upendo usio na mipaka. Na siku tukiwapoteza ni huzuni kubwa sana kama mti mkubwa ulio kwenye uwanda mkavu, ukiwa umesimama peke yake. Mizizi yake inajitahidi kufikia maji ya kumbukumbu, lakini udongo wa upweke hauna rutuba. Majani yamekauka, na kila tawi lililokatika ni kama upotevu mwingine, huku mti ukisimama peke yake, ukijaribu kuishi licha ya maumivu hayo yote ni kwa sababu huzuni ni mwendelezo wa kawaida wa upendo.
Huzuni ni taa kubwa ya neon, yenye mwanga mkali inayoonekana kila mahali, ikionyesha kila sehemu, ikitangaza kwa sauti kubwa, 'Upendo ulikuwa hapa.' na kwa maandishi madogo,'Upendo bado upo'.
Ndugu yangu hakika msiba usikie kwa jirani ila usiombae ukufike; maana ni afadhali kusikia juu ya matatizo au misiba inayowapata watu wengine (jirani), lakini unapaswa kuomba na kutarajia kwamba misiba hiyo isikufike au isikupate wewe mwenyewe.
Japo muda mwengine huo msemo unaokena una ukakasi ila naamini unatoa wito mkubwa wa kuwa na huruma na kuelewa maumivu ya wengine wakati huo ukitamani na kuomba kwamba wewe mwenyewe usipatwe na hali kama hiyo. Hii inaonyesha ukweli kwamba msiba ni kitu kibaya,kinaumiza sana ila kwa waamini tunajua ndiyo njia ya kukutana na Mola wetu Jalia na ingawa tunaweza kushiriki huzuni na wengine, ni jambo ambalo hakuna mtu anayetamani kumkuta. Bora uwe kwenye nafasi ya kufariji kuliko kufarijiwa; unayetoa kuliko kupokea.
Ila kama tujuavyo, Mola wetu sio utaratibu wake – na hafanyi kama fahamu za binadamu zinavyotaka; siku zote humuita yeyote anayemtaka; hajali mdogo wa rika au mkubwa wa rika; Rais au raia; tajiri au masikini; fukarafuke au hoehae; una kaa Masaki au Madongoporomoka; mnyonge au jasiri – yeye akikutaka atakuita tu.




